Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza (mwenye tisheti nyeupe katikati) akiwa katika mazoezi ya jogging na kikundi cha Kawe Jogging Social Club katika sherehe za miaka mitano ya kikundi hicho zilizofanyika leo jijini Dar es Salaam (aliyenyoosha kidole kushoto) ni Katibu wa Kawe Jogging Social Club Bw.Alhaj Seif Muhere.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza (mwenye tisheti nyeupe katikati)akifanya mazoezi ya viungo na wanachama wa vikundi mbalimbali vya jogging mkoani Dar es Salaam katika sherehe za miaka mitano ya kikundi cha Kawe Jogging Social Club leo,(kushoto) Katibu wa Kawe Jogging Social Club Bw.Alhaj Seif Muhere na kulia ni Mwanachama wa Jogging Kawe Social Club Bi Felister Mwijage.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza akizungumza na wanachama wa vikundi mbalimbali vya jogging Mkoani Dar es Salaam katika sherehe za maadhimisho ya miaka mitano ya kikundi cha Kawe Jogging Social Club zilizofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Na Anitha Jonas – WHUSM

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ametoa wito kwa vijana kujiunga na vikundi vya mazoezi maarufu kama (Jogging Club) kwa ajili ya kuimarisha afya zao na kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa wito huo katika sherehe za maadhimisho ya miaka mitano ya Kawe Jogging Social Club zilizofanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo aliwapongeza wanachama wa Klabu hiyo kwa kuweza kudumu kwa muda wote huo.

“Napenda kuwapongeza kwa juhudi zenu pamoja na ubunifu mliyoutumia katika kujiongezea kipato kupitia klabu yenu kwa kuanzisha mgahawa ambao unawaongezea kipato na kukuza uchumi wenu kwa hakika mmekuwa ni mfano wa kuigwa,”Mhe. Shonza.

Akiendelea kuzungumza katika sherehe hizo Naibu Waziri huyo amewahakikishia wanaklabu hao ushirikiano pamoja na kushughulikia maombi yao ya kupatiwa mashine ya maximalipo.

Naye Mwenyekiti wa Kawe Jogging Social Club Bw. Abdul Risasi alimshukuru Naibu Waziri kwa kujumuika nao katika sherehe hiyo na kutoa ombi la kusaidiwa kupata mfadhili atakayeweza kuwasaidia kufanikisha ushiriki wao katika mashindano ya Kilimarathon yanayotarajia kufanyika Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro.

“Tumekuwa tunashiriki katika mashindano ya Kilimanjaro Marathon kwa miaka minne mpaka sasa na Kawe Jogging Social Club imekuwa ndiyo kikundi pekee nchi nzima ambacho kimepata nafasi ya kuweza kushiriki mashindano hayo ambapo wanachama wake hukimbia mpaka kilometa 21,”alisema Bw.Risasi.

Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo aliendelea kutoa wito kwa vijana kujiunga katika vikundi vya jogging kwani kupitia umoja huo wanaweza kujitengeneza fursa za kiuchumi na kujiongezea kipato badala ya kukaa vijiweni na kulalamikia hali ngumu ya maisha.

Kwa upande wa mmoja wa wanachama wa Msasani Jogging Club Bi Asha Said alitoa maoni yake na kusema jogging clubs ni nzuri kwani zinasaidia kupata marafiki pamoja na kuimarisha afya.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...