THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

UUZWAJI WA VIWANJA ENEO LA MADAGANYA MOROGORO MJINI


MICHUZI TV LIVE: RAIS DKT MAGUFULI AKIWATUNUKU VYETI WAJUMBE WA KAMATI YA MAKINIKIA, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM LEO


MHASHAMU BABA ASKOFU MAPUNDA AHIMIZA JUU YA UMUHIMU WA KUJITEGEMEA WENYEWE NA KUONDOKANA NA TABIA YA UTEGEMEZI

Mhashamu Baba Askofu Jimbo Katoliki Singida,Edward Mapunda akiongoza misa ya ibada ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuzaliwa kwa Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni iliyofanyika katika viwanja vya kanisa hilo mjini Manyoni.

Na Jumbe Ismailly, MANYONI.

MHASHAMU Baba Askofu Jimbo Katoliki Singida,Edward Mapunda amewataka waumini wa madhehebu hayo kuondokana na tabia ya kutegemea wafadhili wakati wa utekelezaji na ukamilishaji wa miradi mbali mbali ya maendeleo na kuwataka watambue kuwa bwana bure amekufa na aliyebakia kwa sasa ni bwana kujitegemea peke yake. Mhashamu Baba Askofu ametoa wito huo kwenye misa takatifu aliyoiongoza wakati wa maadhimisho ya sherehe za Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni iliyofanyika katika viwanja vya Kanisa la Parokia hiyo mjini Manyoni.

“Lakini ninachotaka kusisitiza jambo moja la kujitegemea,jambo moja la kujitegemea..enh tumesikia wazee wetu hapa walichanga hela,wazee wetu walichanga hela….wazeeeeee mlichanga hela sasa na sisi tunataka kuchanga hela ninyi mbona mlichanga tunataka kujenga Parokia.”alisisitiza baba Askofu Mapunda.
baadhi ya viongozi wa Parokia jimbo Katoliki Singida wakiwa katika maandamano ya kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu kuzaliwa kwa Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni kwenye sherehe za maadhimisho hayo yaliyofanyika mjini,Manyoni.

Aidha Kiongozi huyo mkuu wa Kanisa hilo alisisitiza kwa wakazi wa wilaya ya Manyoni kwamba suala la kujitegemea halina budi kupatiwa kipaumbele katika shughuli za kukamilisha ujenzi wa majengo ya makanisa pamoja na vigango. Akifafanua zaidi Baba Askofu huyo aliweka bayana kuwa jukumu la kukamilisha ujenzi wa makanisa ni la waumini wenyewe na wenye moyo ambapo hata hivyo aliwatoa hofu waumini wa Manyoni kwa kuweka wazi msimamo wake kuwa anaamini kabisa waumini wa Manyoni ni waumini wenye moyo wa dhati wa kukamilisha majengo hayo.

Kutokana na moyo huo walionao wana Manyoni,Baba Askofu huyo alitumia wasaa wa maadhimisho hayo ya miaka 50 ya Jubilee kwa kuwataka waumini wa Jimbo hilo la Manyoni wajitoe bila kujibakiza,ili mipango na mikakati waliyojiwekea katika Jubilee hiyo iweze kufanikiwa zaidi.

“Namkumbuka sana Askofu Balina,askofu Balina alikuwa wa jimbo Katoliki la Shinyanga tunamuombea kwa Mungu ametangulia kwa Mungu lakini alikuwa anawaambia wasukuma wenzake maneno mazuri sana,na mimi nataka niwaambie hayo wana Manyoni kwa sababu mikakati hii ni mizito,mipango hii ni mizito,maazimio haya ni mazito tusipojitoa yote yatakwama”alisema huku akishangiliwa na waumini.


baadhi ya waumini wa kanisa hilo waliohudhuria kuadhimisha miaka 50 tangu kuzaliwa kwa Parokia ya Kupaa Bwana Manyoni,iliyofanyika mjini Manyoni.Picha zote Na Jumbe Ismailly.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa madhehebu ya Kikatoliki askofu Banila alikuwa akiwaambia wanashinyanga kwamba bwana bure amekufa na kwa kutokana na kauli hiyo naye Baba Askofu Mapunda alitumia pia kauli hiyo kwa kuwaasa waumini wa jimbo hilo kwamba bwana bure amekufa na bwana misaada yupo taabani na hivyo aliyebakia ni bwana kujitegemea.
Hata hivyo Askafu Mapunda aliwatahadharisha waumini wa jimbo hilo kwamba suala la kujitegemea lina umuhimu wake na kwa hali hiyo hawana ujanja wa kulikwepa jukumu hilo la kuondokana na utegemezi na kwenda kwenye tabia ya kujitegemea wenyewe kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili Mapadrii zikiwemo changamoto za kutokuwa na vyombo vya usafiri.

Naye Paroko wa Parokia  ya Kupaa bwana Manyoni Jimbo Katoliki Singida,Padri Thomasi Wambura  alisema mwaka jana ulikuwa mwaka wa Jubilee ya 100  wa Mapadri Tanzania mwaka huu wao nao wanaadhimisha miaka 50 ya Jubilee ya Parokia yao na mwaka ujao wa 2018 wataadhimisha Jubilee ya miaka 150 tangu ukristo ulipoingia nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Padri Wambura waumini wote wana wajibu wa kuyatekeleza yale yote waliyoaswa na Baba Asskofu kama mchungaji wao mkuu lakini hakusita kusisitiza kwamba wajibu walionao ni kuyatekeleza yale waliyoyapata katika ukrito. Kwa upande wao baadhi ya waumini wa Kanisa hilo,Elizabeth Mkyalu  alishauri kwamba fedha zilizochangwa na waumini wa kanisa hilo hazina budi kuanza shughuli zilizokusudiwa za ujenzi wa majengo hayo huku akionya tabia ya kusubiri wafadhili kwamba kwa namna moja au nyingine hukwamisha miradi iliyoanzishwa pale wanapojitoa au kutochangia.

Naye Flora Lyimo kwa upande wake alisema kwamba njia pekee ya kujikwamua kiuchumi na kijamii na kuhakikisha maeendeleo endelevu yanapatikana ni kujiamini na kusimama wenyewe kwa miguu yao na siyo kusubiri kusaidiw a na watu wengine kwani endapo watasubiri misaada upo uwezekano wa malengo waliyojiwekea kutokamilika.


SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA ZA KISHERIA WALE WOTE WANAOANZA KUJENGA MIJINI KWENYE MAENEO YASIYOPIMWA NA BILA VIBALI VYA UJENZI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen wakati walipoenda kutatua mgogoro wa ardhi wa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, ambapo ameagiza eneo hilo lirejeshwe serikalini.

Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Serikali kuanzia sasa imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuvunja majengo yote yanayoanza kujengwa katika miji yao bila ya kibali na yale yanayojengwa kwa dhuruma na watu wasio na hati katika viwanja vya watu wengine walio na hati miliki zao za ardhi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameyasema hayo alipofanya ziara wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alipoenda kutatua mgogoro wa ardhi ambapo ameagiza eneo ya lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa umekiukwa kwa kiwango kikubwa, na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa kabisa.

Waziri Lukuvi amesema tatizo la ujenzi holela lianaanza pale ambapo Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wanawaacha majengo yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndio anayejenga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji na kuwaagiza kuweka alama za x na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati za kumiliki ardhi kwa dhuruma.

“japokuwa serikali inaendelea na kurasimisha maeneo, Hatuwezi kuendelea na zoezi la kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana, kwa hiyo naagiza kuanzia sasa Wakurugenzi, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuondoa majengo yote yanayoanza kujengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa na watu wanaodhulumu viwanja vya watu masikini” amesema Lukuvi.

 *Lukuvi amesema atapambana na viongozi ambao wataruhusu watu wasio na hati za kumiliki ardhi kujenga katika viwanja vya wamiliki wengine wenye hati zao.*

Waziri Lukuvi amezitaka Halmashauri zote nchini kutoa vibali vya ujenzi katika muda mfupi na kutenga viwanja vingi vilivyopimwa ili kuwapa fulsa wananchi kujenga katika maeneo yaliyopimwa na yaliyopangwa vizuri katika miji yao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemhakikishia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwa atayafanyia kazi mapendekezo yake kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa wake katika masuala yote ya ardhi.
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.

Aidha, katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema Serikali imekusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliokopeshwa kwa kuyatumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo hawaitumii kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi waliyoitumia kama dhamana.

Waziri Lukuvi ameongeza kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa kutumia ardhi kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo wanaitumia kuwekeza nje ya nchi na kujenga majengo nchi za Ulaya, dubai na kwingine duniani.

Lukuvi amesema Haiwezekani mtu atumie ardhi yetu kujipatia fedha halafu fedha hizo azitumie kuendeleza nchi nyingine na kuiacha ardhi yetu kama pori jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo.
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.

“Kwa hiyo Wizara yangu imekusudia mwezi ujao kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria namba 4 ya mwaka 1999 ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana” amesema Waziri Lukuvi.

Marekebisho haya tunalenga kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mikopo iliyotolewa itumike kuendeleza sehemu ya ardhi husika iliyotumika kama dhamana ya kuomba mkopo katika mabenki. Kwa kuwa Tathmini iliyopo inaonesha, baada ya wekezaji hao kupata mikopo kwa kutumia ardhi kama dhamana fedha hizo hawazitumii kuendeleza ardhi husika au katika uwekezaji wowote hapa nchini.

Lukuvi amesema, kuanzia mwezi Novemba tatizo hilo litakwisha kabisa kwa kuwa jukumu hili yatapewa mabenki na wakopeshaji wote ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika Benki husika.

“na kama Benki husika haitowafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, basi Serikali itamyang’anya mkopeshwaji huyo shamba hilo kwa kuwa atakua amekiuka sheria halafu Benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleza shamba lile itakuwa imekula hasara yenyewe” amesema Waziri Lukuvi.


BREAKING NYUZZZZ......: RAIS DKT. MAGUFULI AMTEUA PROF. FLORENS LUOGA KUWA GAVANA WA BENKI KUU YA TANZANIA

Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ametangaza kuteua Profesa Florens Luoga kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania akipokea kijiti kutoka kwa Gavana wa awali, Profesa Benno Ndulu. Rais Dkt. Magufuli ametangaza uteuzi huo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyeti kwa Kamani ya zilizofanya uchunguzi wa kiwango, aina na thamani ya madini katika makinikia yaliyopelekea mazungumzo na Kampuni ya Barrick Gold. Profesa Luoga alikuwa ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati hiyo.


Dkt. Kigwangalla afuta vibali vyote vya uwindaji kwa makampuni nchini

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla amefuta vibali vyote vilivyotolewa na Wizara yake vya Uwindaji wa makampuni ili kuwa na utaratibu mpya wa uombaji kwa njia ya mnada.

Waziri Dk.Kigwangalla ametoa agizo hilo jana jioni wakati wa kuhitimisha mazungumzo yake na wadau mbalimbali wa sekta ya Utalii na Maliasili aliokutana nao mjini hapa Dododma.

“Kwa mamlaka niliyonayo. Natamka kwamba, nafuta rasmi vibali vyote vya Uwindaji kwa makampuni vilivyotolewa na wizara yangu kwa mwaka huu. Pia naagiza Watendaji wote wanaosimamia ili, wahakikishe wanaandaa mchakato ndani ya siku 60 ili mchakato huo wa mnada ufanyike na uwe wa uwazi” alieleza Dkt. Kigwangalla.

Pia ametoa onyo na maagizo mazito kuhakikisha kuwa vitalu vyote vyenye migogoro ikiwemo vile vya Loliondo, Natroni na maeneo mengine kutotolewa kwa vibali vya uwindaji mpaka hapo watakapokamilisha tatizo la migogoro hiyo.
Aidha, ametoa agizo kwa hoteli 10 zilizobinafsishwa kutoka Serikalini zirejeshwe ndani ya siku 60 kuanzia sasa huku akiagiza watendaji waandike barua kwa msimamizi wa hazina.


UNNEWSKISWAHILI KWA HABARI YA KILA SIKU KUTOKA IDHAA YA KISWAHILI YA UMOJA WA MATAIFA


Naibu Waziri Shonza:Vijana jiungeni na vikundi vya Mazoezi

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza (mwenye tisheti nyeupe katikati) akiwa katika mazoezi ya jogging na kikundi cha Kawe Jogging Social Club katika sherehe za miaka mitano ya kikundi hicho zilizofanyika leo jijini Dar es Salaam (aliyenyoosha kidole kushoto) ni Katibu wa Kawe Jogging Social Club Bw.Alhaj Seif Muhere.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza (mwenye tisheti nyeupe katikati)akifanya mazoezi ya viungo na wanachama wa vikundi mbalimbali vya jogging mkoani Dar es Salaam katika sherehe za miaka mitano ya kikundi cha Kawe Jogging Social Club leo,(kushoto) Katibu wa Kawe Jogging Social Club Bw.Alhaj Seif Muhere na kulia ni Mwanachama wa Jogging Kawe Social Club Bi Felister Mwijage.
Naibu Waziri wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Juliana Shonza akizungumza na wanachama wa vikundi mbalimbali vya jogging Mkoani Dar es Salaam katika sherehe za maadhimisho ya miaka mitano ya kikundi cha Kawe Jogging Social Club zilizofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Na Anitha Jonas – WHUSM

Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza ametoa wito kwa vijana kujiunga na vikundi vya mazoezi maarufu kama (Jogging Club) kwa ajili ya kuimarisha afya zao na kujikwamua kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa wito huo katika sherehe za maadhimisho ya miaka mitano ya Kawe Jogging Social Club zilizofanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo aliwapongeza wanachama wa Klabu hiyo kwa kuweza kudumu kwa muda wote huo.

“Napenda kuwapongeza kwa juhudi zenu pamoja na ubunifu mliyoutumia katika kujiongezea kipato kupitia klabu yenu kwa kuanzisha mgahawa ambao unawaongezea kipato na kukuza uchumi wenu kwa hakika mmekuwa ni mfano wa kuigwa,”Mhe. Shonza.

Akiendelea kuzungumza katika sherehe hizo Naibu Waziri huyo amewahakikishia wanaklabu hao ushirikiano pamoja na kushughulikia maombi yao ya kupatiwa mashine ya maximalipo.

Naye Mwenyekiti wa Kawe Jogging Social Club Bw. Abdul Risasi alimshukuru Naibu Waziri kwa kujumuika nao katika sherehe hiyo na kutoa ombi la kusaidiwa kupata mfadhili atakayeweza kuwasaidia kufanikisha ushiriki wao katika mashindano ya Kilimarathon yanayotarajia kufanyika Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro.

“Tumekuwa tunashiriki katika mashindano ya Kilimanjaro Marathon kwa miaka minne mpaka sasa na Kawe Jogging Social Club imekuwa ndiyo kikundi pekee nchi nzima ambacho kimepata nafasi ya kuweza kushiriki mashindano hayo ambapo wanachama wake hukimbia mpaka kilometa 21,”alisema Bw.Risasi.

Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo aliendelea kutoa wito kwa vijana kujiunga katika vikundi vya jogging kwani kupitia umoja huo wanaweza kujitengeneza fursa za kiuchumi na kujiongezea kipato badala ya kukaa vijiweni na kulalamikia hali ngumu ya maisha.

Kwa upande wa mmoja wa wanachama wa Msasani Jogging Club Bi Asha Said alitoa maoni yake na kusema jogging clubs ni nzuri kwani zinasaidia kupata marafiki pamoja na kuimarisha afya.


WASHINDI WA AFYABANDO WA DROO YA TATU WAPATIKANAMtaalam wa Tehama wa Nordic Foundation Tanzania Dickson Leonard (katikati) akibadilishana mawazo na Mkaguzi kutoka Bodi ya Taifa ya Michezo ya kubahatisha, Emmanuel Ndaki (kushoto) na Mkurugenzi mwendeshaji wa Kampuni ya Bima ya Zurich Group/ Jubilee wakati wa zoezi la kuendesha kampeni ya Afyabando ya tatu kuwapata washindi 10 watakaokabidhiwa kadi za Bima ya afya kwa ajili ya matibabu pamoja na familia. Mchezo huo umechezeshwa jijini Dar es Salaam Oktoba 22. 2017. (Imeandaliwa na Robert Okanda Blogs)

Mtaalam wa Tehama wa Nordic Foundation Tanzania Dickson Leonard (kulia) akiwasiliana na mmoja wa washindi wa kampeni ya Afyabando ambapo washindi 10 watakaokabidhiwa kadi za Bima ya afya kwa ajili ya matibabu pamoja na familia. Mchezo huo umechezeshwa jijini Dar es Salaam Oktoba 22. 2017. Kushoto ni Mkaguzi kutoka Bodi ya Taifa ya Michezo ya kubahatisha, Emmanuel Ndaki.

Mtaalam wa Tehama wa Nordic Foundation Tanzania Dickson Leonard (kulia) akiwasiliana na mmoja wa washindi wa kampeni ya Afyabando ambapo washindi 10 watakaokabidhiwa kadi za Bima ya afya kwa ajili ya matibabu pamoja na familia. Mchezo huo umechezeshwa jijini Dar es Salaam Oktoba 22. 2017. Kushoto ni Mkaguzi kutoka Bodi ya Taifa ya Michezo ya kubahatisha, Emmanuel Ndaki.

Mtaalam wa Tehama wa Nordic Foundation Tanzania Dickson Leonard (kulia) akibonyeza kitufe kuwapata washindi wa kampeni ya Afyabando ambapo washindi 10 watakaokabidhiwa kadi za Bima ya afya kwa ajili ya matibabu pamoja na familia. Kushoto ni Mkaguzi kutoka Bodi ya Taifa ya Michezo ya kubahatisha, Emmanuel Ndaki. 


BREAKING NYUZZZZZ: MAHAKAMA YAMKUTA LULU NA KESI YA KUJIBU KUHUSU KIFO CHA KANUMBA

Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam leo Oktoba 23, 2017 imemkuta Msanii maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael Maarufu kama Lulu, anakesi ya Kujibu.

Ni kuhusu tuhuma zinazomkabili za kumuua msanii mwenzake, marehemu Steven Kanumba ambaye pia alikuwa ni mpenzi wake, April 6 mwaka 2012.
Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao kwa kuita mashahidi wanne.

Kesi imeahirishwa hadi saa tano kamili ambapo Lulu ataanza kujitetea.


Tanzania yatwaa taji la Cana kanda ya tatu kwa mara ya pili mfululizo

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza akimkabidhi kombe nahodha wa Tanzania, Sonia Tumiotto pamoja a Natalie Sanford mara baada ya kutwaa ubingwa wa Cana Kanda ya Tatu.

Tanzania imefanikiwa kutetea ubingwa wa Cana Kanda ya Tatu Afrika baada ya kuibuka katika nafasi ya kwanza katika upande wa wanawake na wanaume. Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa juzi, timu ya Tanzania ilipata jumla ya pointi 1,394 na kufanikiwa kuzishinda timu maarufu na kali katika mchezo huo, Zambia ambayo ilipata pointi 968 na Kenya iliyomaliza ya tatu kwa pointi 957.

Uganda ambayo ndiyo nchi ya kwanza kuandaa mashindano hayo, ilimaliza ya nne kwa kupata pointi 759 na kufuatiwa na Afrika Kusini iliyopata pointi 469 ma Sudani iliyopata oint 459 katika mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Vodacom Tanzania, Swissair, JCDecaux, Coca Cola, Label Promotions, Tanzania Sign Writers, Giraffe Ocean View, Print Galore na Slipway Hotel. 

Katika mashindano hayo ya siku tatu, timu ya wanawake wa Tanzania ndiyo ilikuwa kali zaidi kutokana na kuundwa na waogeleaji nyokta kama Sonia Tumiotto ambaye ndiye nahodha na Natalie Sanford. Mbali ya hao kulikuwa na nyota wengine kama Maia Tumiotto ambaye anakuja juu kwa kasi, Smriti Gorkan, Kayla Gouws, Amani Doggart, Tara Behnsen, Emma Imhoff, Rania Karume , Chichi Zengeni, Anjani Taylor, Anna Guild, Sanne Kleinveld , Angelica Spence, na Tami Triller.

Kwa upande wa wanaume , nyota alikuwa Marin De Villard pamoja na wakali wengine kama Collins Saliboko, Joseph Sumari, Denis Mhini, Hilal Hilal, Adil Bharmal, Judah Miller, Elia Imhoff, Delvin Barick, Caleb O'Sullivan, Khaleed Ladha, Matthew Guild , Chris Fitzpatrick, Harry McIntosh, Dhashrrad Magesvaran na Joseph Sumari.

Kwa upande wa timu ya Platnum, nayo ilionyesha kuwa kuna nyota wa baadaye wa Tanzania ambapo timu ya wanawake iliindwa na Shivan Bhatt, Natalia, Charlotte Sanford, Vanessa Dickson ), Rebecca Guild, Meredith Boo , Maria Bachmann ), Kayla Temba na Maya Somaiya.

Kwa wanaume walikuwa Aravind Raghavendran, Mohameduwais Abdullatif (Bluefins), Abraham Kayugwa, Terry Tarimo, Aliasgar Chakera, Zeke Boos , Yuki Omari, Augustino Lucas , Fallih Ahmed, Carter Helsby , Ian Lukaza na Emmanuel Stenson. Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza aliwapongeza waogeleaji wa Tanzania kwa kutwaa ubingwa huo huku akiahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa chama cha kuogelea cha Tanzania (TSA).
Waogeleaji wa timu ya Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutetea vyema ubingwa wa Cana kanda ya tatu.
Muogeaji nyota wa Tanzania, Sonia Tumiotto akipigania Taifa lake katika mashindano ya Cana kanda ya tatu.
Collins Saliboko wa Tanzania akishindana katika mashindano ya Cana Kanda ya Tatu Afrika.
Makocha wa timu ya Tanzania wakishangilia mara baada ya kutwaa ubingwa wa Cana Kanda ya Tatu kwa mchezo wa kuogelea.


VIDEO: DKT. HARRISON MWAKYEMBE ASHEREHEKEA NA WAHINDU MWAKA MPYA WA KIHINDU WA 2074 JIJINI DAR ES SALAAM


MABARAZA YA MADIWANI SIMIYU YARIDHIA HALMASHAURI ZIKOPE BILIONI 17.1 KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (katikati) akizungumza na Madiwani na baadhi ya wakulima Bonde la Mwamanyili wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega (hawapo pichani) katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani, kilichofanyika Nyashimo kwa lengo la kujadili suala la maombi ya mkopo kwa ajili kutekeleza Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili Wilayani humo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mhe.Vumi Magoti(wa pili kulia)akizungumza na Madiwani na baadhi ya wakulima wa Busega(hawapo pichani) katika kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Nyashimo kwa lengo la kujadili maombi ya mkopo kwa ajili kutekeleza Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili Wilayani humo
Madiwani na baadhi ya Wafugaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu wakifuatilia mjadala kuhusu suala la maombi ya Mkopo kwa ajili ya Upanuzi wa Kiwanda cha Maziwa Wilayani Meatu katika kikao cha dharura cha Baraza kilichofanyika Mjini Mwanhuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Busega (meza kuu) na baadhi ya wakulima baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwa lengo la kujadili suala la maombi ya mkopo kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili wilayani humo.

Na Stella Kalinga, Simiyu
Mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega na Meatu Mkoani Simiyu yameridhia Halmashauri hizo kukopa shilingi bilioni 17.1 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kwa ajili ya kutekeleza Miradi mikubwa miwili ya Maendeleo.

Maridhiano hayo yamefikiwa katika Vikao vya dharura vya mabaraza ya madiwani vilivyofanyika kwa nyakati tofauti, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Busega imepanga kukopa shilingi bilioni 10.7 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mwamanyili (eneo la ekari 2050)  na Meatu shilingi bilioni 6.4 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda cha maziwa(MEATU MILK).

 Akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya Mpango wa Kilimo cha Umwagiliaji Wilayani Busega, Afisa Mipango wa Wilaya hiyo Josephat Joseph, amesema hadi sasa kazi za upimaji wa mashamba na njia ya kupita bomba la maji, kupima udongo, kusanifu mfereji mkuu kwenye chanzo, sehemu ya kuchukulia maji, nyumba za pampu, mifereji ya kuingiza na kutolea maji,kuandaa michoro na gharama za mradi zimeshakamilika.


NYUMBA 58 ZA WATU WALIOVAMIA ENEO LA SHULE YA TABORA WASICHANA ZATEMBEZEWA NYUNDOOZZZ

NA TIGANYA VINCENT, RS-Tabora

MANISPAA ya Tabora kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora imeendesha zoezi la kuwaondoa watu waliovamia eneo la Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora na kufanikiwa kuvunja nyumba zaidi ya 58 za watu waliokuwa wamejenga katika eneo hilo. Hatua hiyo imechukuliwa jana baada ya wahusika kuombwa waondoke kwa hiari kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita lakini walikaidi kutekeleza agizo hilo na kuendelea kuishi katika la Shule hiyo

Akizungumza na waandishi wa habari Mwanasheria kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Richard Lugomela alisema kuwa wavamilizi hao walipewa taarifa ya kuondoka katika eneo shule muda mrefu ambao unazidi mwaka mmoja lakini wamekuwa wakikaidi kuondoka kwa hiari. Alisema kuwa zoezi hilo ambalo limeanzia katika Shule hiyo lina lengo la kuhakikisha maeneo yote ya Taasisi yalivamiliwa yanarejeshwa na yatumika kwa ajili ya maendeleo yao ili  kutoa huduma bora kwa wananchi.

Lugomela aliongeza kuwa hivi sasa ilikuwa ni vigumu kwa Shule kama Tabora wasichana kuweka miundo mbinu zaidi kwa sababu ya kuwepo kwa wavamizi hao. Alisema kuwa wavamizi hao walipewa taarifa na kuomba wapewe muda wa kujiandaa ili waweze kuondoka lakini badala yake wameendelea kukaa kimya na kupuuzia agzio la kuwataka kuondoka katika eneo walilolivamia.

Alitoa wito kwa watu wengine wanaojijua kuwa wamevamia maeneo ya Taasisi nyingine za elimu kama vile Shule ya Sekondari Milambo, Tabora wavulana na hata yasiyokuwa yao kuanza kuondoka wao kwa hiari yao la sivyo watalazimika kulipia gharama za uvunjaji wa nyumba zao endapo Serikali itatekeleza zoezi la kuwaondoa. Lugomela alisema kuwa eneo hilo lilitengwa na Serikali kwa ajili ya matumizi ya Shule ya Wasichana toka mwaka 1958 na pia katika sehemu hiyo lipo eneo ambalo ni chanzo cha maji.

Kwa upande wa Mhandisi wa Maji wa Manispaa ya Tabora Mohamed Almasi alisema kuwa watu waliojenga katika eneo hilo hawana vibali vya ujenzi na hivyo ni wavamili ambao walipaswa kuwa wameshaondoka siku nyingi. Alisema kuwa baada ya kumalizika kwa zoezi la kuwaondoa wavamizi hao katika shule hiyo ya wasichana ya Tabora watahamia katika maeneo mengine ya Taasisi na kwa watu binafsi ambao maeneo yao yamekaliwa na watu wengine kinyume cha sheria.

Almasi alitoa wito kwa wakazi wa Manispaa ya Tabora wanaotaka kujenga wapelekea ramani zao katika Manispaa ya Tabora ili waweze kupatiwa kibali cha ujenzi kabla ya kuendeleza maeneo yao. Mmoja wa waathirika wa bomoa bomoa Hawa Katabi alisema kuwa hakupata taarifa ya zoezi hilo jambo liliwafanya washindwe hata kuondoa mabati na matofauli.

Alisema ni vema zoezi hilo linapotaka kufanyika wakapewa muda wa kutosha ili waweze kuokoa mali zao


Dkt. Abbasi Awapa Siri Tano za Mafaniko Wahitimu Kidato cha Nne Jitegemee

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akimkabidhi cheti cha kuhitimu Kidato cha Nne mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jitegemee ya Jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika Mahafali ya 33 ya Shule ya hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Brigedia Jenerali Mstaafu Lawrence Magere. Kushoto ni Mkuu wa Shule hiyo Luten Kanali Robert Kessy.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akikabidhiwa risala ya wanafunzi wa Kidato cha Nne Shule ya Sekondari Jitegemee ya inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati wa Mahafali ya 33 ya Shule hiyo leo Jijini Dar es Salaaam.
Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akizungumza alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 33 ya Shule ya Sekondari ya Jitegemee inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa leo Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee ya Jijini Dar es Salaam inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Luten Kanali Robert Kessy akizungumza wakati wa mahafali ya 33 ya shule hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule Brigedia Jenerali Mstaafu Lawrence Magere.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiangalia vitabu alipotembelea Maktaba ya Shule ya Sekondari ya Jitegemee ya Jijini Dar es Salaam inayomilikiwa ma Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati wa Mahafali ya 33 ya Shule hiyo leo Jijini Dar es Salaam.


WAZIRI MAKAMBA AKUTANA NA VIONGOZI WA TAASISI ZA MUUNGANO - ZANZIBAR

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. January Makamba leo amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar. Katika kikao hicho kilichofanyika katika Jengo la Uhamiaji Waziri Makamba alitoa fursa ya viongozi hao kuwasilisha maoni na changamoto zinazojitokeza katika utendaji wao wa kazi na kuweka mikakati ya kukabiliana nazo.


KESI YA KUUWA BILA KUKUSUBIA INAYOMKABILI MSANII LULU LUENDELEA LEO MAHAKAMA KUU DAR ES SALAAM

Kesi ya kuuwa bila kukusudia inayomkabili, Msanii wa filamu hapa nchini, Elizabert Michael "Lulu" inaendelea kusikilizwa leo katika Mahakama kuu Dar es salaam, ambapo shahidi wa nne atatoa ushahidi wake Mahakamani hapo. Pichani ni Wakili wa Lulu, Peter Kibatala akijadiliana jambo na mteja wake aliyeambatana na wazazi wake Mahakamani hapo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo. Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia Msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba miaka sita iliyopita. 


RAIS DKT. MAGUFULI KUWATUNUKU VYETI WAJUMBE WA KAMATI ZA MAKINIKIA LEOMAGAZETI YA JUMATATU LEO OKTOBA 23,2017


NEWS ALERT: BARRICK GOLD CORPORATION KUUNDA KAMPUNI MPYA KUENDESHA SHUGHULI ZA UCHIMBAJI MADINI TANZANIA, RAIS MAGUFULI AWA GUMZO DUNIA NZIMA

Barrick Gold Corporation yenye makao yake jijini Toronto, Canada, litaunda kampuni mpya (sio Acacia) kuendesha migodi yake ya Bulyanhuru, Buzwagi na North Mara nchini Tanzania.
Katika taarifa yake juu ya makubaliano na serikali ya Tanzania yaliyofikiwa juzi jijini Dar es salaam, Shirika hilo limesema msimamo wa uwazi ulioafikiwa baina ya washirika (Tanzania na Barrick) ndio utaoainisha namna kampuni hiyo mpya itafanya shughuli zake.
"Kwa mfano Serikali ya Tanzania itashiriki katika maamuzi yahusuyo shughuli, uwekezaji, mipango, manunuzi na masoko (ya kampuni hiyo mpya itapoanzishwa)", sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Makamu wa Rais Mwandamizi  wa Barrick Gold anayeshughulikia Shughuli za Uwekezaji na utawala Bw. Daniel Oh na Makamu wa Rais Mwandamizi wa Barrick anayeshughulikia Mawasiliano Bw. Andy Lloyd.
Taarifa imesema kampuni hiyo mpya itaajili Watanzania, itawajengea uwezo wazawa  katika ngazi zote, kuanzia uanachama wa bodi hadi shughuli zote, na kwamba itaongeza ununuzi wa bidhaa na huduma ndani ya Tanzania katika kuhakikisha faida  ya dhahabu inaifaidisha nchi.
Taarifa hiyo imethibitisha kwamba faida ya kiuchumi kutoka katika migodi hiyo mitatu itagawanwa nusu-kwa-nusu ama 50-kwa-50 baina ya kampuni hiyo mpya na serikali ya Tanzania,  faida yake  ya kiuchumi ikitokana na mirahaba na kodi huku asilimia 16 ikibakia pale pale.
Kupata chanzo na habari kamili BOFYA HAPA

Makubaliano Barrick: JPM awa gumzo duniani
*New York Times wasema ni mageuzi tupu
*Mining Quartz: Ana msimamo usioyumba

SIKU chache tu baada ya Rais John Pombe Magufuli kufanikisha kukamilika kwa ufanisi sehemu ya kwanza majadiliano na kampuni ya Barrick Gold kuhusu biashara ya madini hayo nchini, majarida na magazeti mbalimbali maarufu duniani yamemzungia kwa staili tofauti.

Katika makubaliano hayo, huku Mwenyekiti wa Barrick Gold, Prof. John Thornton, akilazimika kusafiri kwa ndege binafsi kuja mara 2 nchini Tanzania, Tanzania imefikia kile ambacho nchi chache sana duniani zimeweza kufanikisha katika kunufaika na sekta ya madini.

Pamoja na kupewa hisa zinazofikia asilimia 16 katika migodi yote ya Barrick nchini, makubaliano hayo pia yanaruhusu Tanzania kuchukua madini yote yanayopatikana baada ya makinikia kuuzwa na itapata faida ya nusu kwa nusu na Barrick baada ya dhahabu ya kawaida kuuzwa.

Aidha, kampuni ya Barrick itaweka ofisi zake mpya katika jiji la Mwanza Tanzania na kwamba idadi ya watanzania wanaoshiriki katika Bodi na menejimenti ya Shirika hilo itaongezeka ili kulinda maslahi ya pande zote mbili.

Ndio maana katika makala yake iliyoitwa “Tanzania’s squeeze on mining firms seems to be working as it gets $300 million in back taxes” Jarida mashuhuri la masuala ya madini Quartz lilimueleza Rais Magufuli kama kiongozi aliyefanikiwa kuyabana makampuni makubwa kwa maslahi ya wananchi wake na hayumbishwi.

“Rais wa Tanzania mwenye msimamo usioyumba katika madini, Dkt. John Pombe Magufuli anaongoza vita inayohakikisha kuwa makampuni makubwa yanapata haki yao lakini wananchi wa Tanzania nao wanapata faida katika sekta ya madini,” anaandika Abdi Latif Dadir mwandishi wa jarida hilo lenye makao yake makuu Marekani.

Kwa upande wake mtandao wa habari za uchumi na biashara wa Bloomberg ulisema kuwa Rais Magufuli ni kiongozi ambaye “anaifanyia mageuzi makubwa sekta ya madini ili kuwafaidisha wananchi.”

Mtandao huo pia umeongeza kuwa licha ya azma hiyo, Serikali ya Magufuli pia ina mikakati mipana zaidi katika “kutekeleza sera ya viwanda na miradi ya kiuchumi katika nchi ya Tanzania ambayo ni ya sita kuwa na uchumi mkubwa katika Ukanda wa Afrika Kusini mwa Sahara.”

Gazeti mashuhuri la New York Times lilianza kwa kusema Serikali nyingi katika nchi za Afrika na Asia-kutoka Afrika Kusini hadi Indonesia zimeanzisha harakati za kuhakikisha zinafaidika zaidi na madai yao.


Gazeti hilo limeeleza hatua mbalimbali alizozichua Rais Magufuli ikiwemo kuzuia usafirishaji wa mchango wa madini maarufu kama makinikia. “Rais wa Tanzania hata hivyo hakusema iwapo uuzaji nje wa madini hayo utaruhusiwa tena ama la,” limeripoti New York Times.
KAMPUNI YA KILUA INDUSTRIAL GROUP YAANDAA KONGAMANO KUBWA LA UWEKEZAJI WA VIWANDA JIJINI BEIJING,NCHINI CHINA

Kampuni ya Kilua Industrial Group of Companies imeandaa kongamano kubwa la uwekezaji wa Viwanda kwa  kuwaalika viongozi Waandamizi wa Serikali ya Mkoa wa Pwani,wafanyabiashara wakubwa ambao ni wamiliki wa viwanda na makampuni mbalimbali ,litakalofanyika jijini Beijing,nchini China.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo,Mohamed Said Kilua amesema kuwa kongamano hilo linatarajia kufanyika Oktoba 25,2017 katika hoteli kubwa yenye hadhi ya nyota tano jijini Beijing,litakalojumuisha wafanyashabiashara wamiliki wa viwanda na makampuni  wapatao 200 kutoka majimbo mbalimbali nchini China.

“Sisi Kilua Industrial Group of Companies tumeamua  kuibeba dhana ya Tanzania ya Viwanda kwa utekelezaji kwa vitendo,na pia kuunga mkono dhamira ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya Viwanda, na kwa njia moja ama nyingine iweze kuzigeuza rasimali maliasili  kuwa bidhaa”alisema Kilua.

Tanzania iliyojaaliwa ardhi yenye rutuba kwa kilimo cha mazao ya Chakula na Biashara,haiwezi kutafsiri maendeleo hayo ya Kilimo bila kuzigeuza bidhaa zilizoandaliwa kwa soko la ndani na lile la Kimataifa bila kuwepo na viwanda vidogo/vya kati na vikubwa vitakavyozalisha bidhaa zenye viwango vyenye ubora katika ushindani wa soko”alisisitiza Kilua.
 Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni Kilua Industrial Group of Companies,Mohamed Said Kilua (pichani shoto) pamoja na viongozi waandamizi wa Serikali ya mkoa wa Pwani wakipatiwa maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Huateng Metalluargical Co.Ltd, Chunsheng Jiang (wa nne kulia) kuhusiana na michoro waliyopewa kama zawadi, ikionesha mandhari ya maeneo mbalimbali ya jiji la Beijing pamoja na shughuli zao nchini China,kabla ya kupata chakula cha pamoja usiku huu, Oktoba 22,2027.

Viongozi hao ni Mkurugenzi wa halmashauri Wilaya ya Kibaha, Bi. Tatu Selemani (kofia nyekundu), Mansouly Ally ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibaha, Afisa Biashara (M) Pwani Suleiman Sirindwa, Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji -Mkoa wa Pwani,Shangwe Twamala, Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bi. Philomena Kasanga pamoja na Katibu Tawala mkoa wa Pwani, Zuberi Mhina. 

Viongozi hao wamekuja jijini Beijing nchini China kwa ziara iliyoratibiwa na Kampuni ya Kiluwa Group of Companies,chini ya Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wake Mohamed Said Kiluwa (mwenye koti la njano) kwa ajilia kushiriki Kongamano kubwa la Viwanda. 
Aidha baada ya kukutana leo viongozi hao pamoja na wadau wakuu wa mambo ya viwanda nchini China, ambapo Oktoba 25 kutakuwepo na Kongamano litakalohusu masuala ya viwanda,litakajumuisha wadau wapatao 200 kutoka maeneo mbalimbali nchini humo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani (pichani kati)Zuberi Mhina akikata kipande cha nyama ya Mbuzi,ikiwa ni ishara ya kuwakaribisha wageni na wenyeji kwenye chakula cha jioni kiliochoandaliwa na wenyeji wa Beijing,kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni Kilua Industrial Group of Companies,Mohamed Said Kilua,kulia ni Katibu Tawala Msaidizi - Uchumi na Uzalishaji -Mkoa wa Pwani,Shangwe Twamala pamoja na Katibu wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Bi. Philomena Kasanga wakishuhudia tukio hilo usiku huu.
 Baadhi ya wenyeji ambao nao wanatarajiwa kushiriki kongamano la Viwanda linalotarajia kufanyika Octoba 25,2017 chini ya Uratibu mkubwa wa kampuni ya Kilua Industrial Group of Companies,jijini Beijing nchini China.
 Wageni wakipewa maelezo mafupi katika baadhi ya michoro ambayo walipewa kama zawadi kutoka kwa wenyeji wao,kabla ya kupata chakula cha jioni pamoja.


MWENYEKITI WA KITONGOJI AVULIWA UONGOZI NA WANANCHI MWINGINE AJIUZULU MBELE YA DC MTATURU

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza na wananchi wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.


Na Mathias Canal, Singida

Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Kazizi Ndg Kurwa Maduka amevuliwa uongozini na Wananchi Wakati wa Mkutano wa hadhara kutokana na tuhuma za kuruhusu na kuingiza wavamizi katika hifadhi ya msitu zinazomkabili huku wananchi hao wakipendekeza Aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Ndg Mussa Mkumbo kuendelea Kuhudumu katika nafasi hiyo.

Mkutano huo uliofanyika katika eneo la Ofisi ya Kijiji Cha Mtavira na kuhudhuriwa na wananchi 353 kutoka Kijiji Cha Makilawa, Mtavira na Mteva Kata ya Makilawa umepelekea pia Mwenyekiti wa Kijiji Cha Mtavira Ndg Jilala Lutelemula kujiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali zinazomkabili ikiwemo tuhuma za kuchukua Rushwa ili kuwaacha wafugaji waendelee kuishi na kuharibu msitu.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akizungumza na wananchi wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.

Mara Baada ya Mwenyekiti huyo kujiuzulu katika Mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu Aliagiza kuitishwa Mkutano wa wananchi haraka iwezekanavyo ili kuchagua Mwenyekiti mpya ambapo pia ameagiza Mwenyekiti huyo kutiwa nguvuni ili kulisaidia Jeshi la polisi kubaini wahujumu wa msitu huo.

Mhe Mtaturu pia aliliamuru Jeshi la polisi kumtafuta popote alipo aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Kazizi Ndg Kurwa Maduka kutokana na tuhuma zinazomkabili ikiwemo kuzuia wananchi kuhama katika msitu huo Jambo ambalo Ni kosa kisheria.

Usiku wa kuamkia Octoba 17, 2017 Mhe Mtaturu aliongoza Kamati ya ulinzi na usalama Wilaya ya Ikungi kuwasaka na kuwakamata wavamizi wa msitu wa Minyughe wanaoendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo Makazi, kilimo na Ufugaji kinyume na Tangazo la serikali (GN) ya kuanzisha hifadhi ya msitu wa Minyughe ya Mwaka 2007.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mtavira, Makilawa na Mteva wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Ofisi za serikali za kijiji cha Mtavira.

Katika Oparesheni hiyo Kamati ya ulinzi na usalama pamoja na mambo mengine pia iliyobaini ukiukwaji wa taratibu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Vijiji na Vitongoji ikiwemo kuwauzia mavamizi maeneo kwa kutoa Rushwa ya fedha au Mifugo.


ZANZIBAR INAENDELEA KUUNGWA MKONO NA MATAIFA YA KIGENI DUNIANI - SMZ
Na Ismail Ngayonga, MAELEZO - ZANZIBAR
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetoa hofu wananchi na kuwaeleza kuwa mataifa mbalimbali duniani yanaendelea kuunga mkono na kutoa ushirikiano mkubwa kwa Rais Dkt. Ali Mohamed Shein katika jitihada mbalimbali zake za kuwalelea maendeleo Wazanzibar.
Hayo yamesemwa leo (Jumamosi Oktoba 21, 2017) Mjini Zanzibar na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Gavu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathimni ya ziara ujumbe wa Mfalme wa Oman, Qaboos bin Said Al-Said aliyetembelea Zanzibar tarehe 22 Septemba mwaka huu.
Gavu alisema katika kudhihirisha kuimarika kwa uhusiano na mataifa mbalimbali duniani, Serikali ya Zanzbar tayari imepokea mialiko tisa ya ziara za nje ya nchi zinazotarajiwa kufanywa na Rais Dkt. Ali Mohamed Shein na Viongozi wa Serikali kuanzia mwishoni mwa mwezi Januari 2018.

“Serikali inaendelea kupanua wigo wa ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa ya kigeni, hakuna haja ya wananchi kuwa na hofu, na tutaendelea kukaribisha ushirikiano na mataifa ya nchi jirani kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya wananchi wetu” alisema Gavu
Gavu alisema tangu kuingia madarakani kwa Rais Shein, Novemba 2015 uhusiano wa Zanzibar na mataifa mbalimbali ulimwengu umekuwa ukiimarika na kueleza kuwa Kiongozi tayari amesafiri katika mataifa ya Djibout, Morroco na Commoro.
Aidha Gavu alisema katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na nchi marafiki, nchi ya Saudi Arabia inatarajia kufungua Ofisi ndogo ya Ubalozi Zanzibar na hivyo kuwataka Wananchi wa Zanzibar kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali yao ikiwemo kudumisha amani, umoja na mshikamano.
Akizungumzia kuhusu ziara ya Mfalme Qaboos bin Said Al-Said wa Oman aliyoifanya Zanzibar hivi karibuni, Serikali ya Zanzibar tayari imeunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya mfalme wa Oman na Rais Shein.
Aliongeza kuwa katika ziara hiyo, Mfalme wa Oman alikubali kutoa ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wanafunzi wa wanafunzi wa Zanzibar katika masuala ya mafuta na gesi pamoja na kujenga viwanda vya kusindika samaki.

“Tutahakikisha kuwa tunapeleka vijana wenye sifa na weledi katika masomo hayo ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inatumia vyema fursa hiyo, ambapo kwa kuanzia hivi sasa wapo wanafunzi wa masomo hayo katika nchi ya China wakipata ujuzi wa tasnia ya mafuta” alisema Gavu.

Wakati wa ziara ya ujumbe wa Oman, Waziri Gavu alieleza kuwa katika mazungumzo ya ya ujumbe huo na Rais Shein, Mfalme Qaboos bin Said Al-Said alikubali pia kufanya matengenezo makubwa ya jengo la Beit –el Ajab pamoja na jengo la “People’s palace”, hatua inayolenga kuimarisha ukuaji wa sekta ya utalii Zanzibar.

Kwa upande wake Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masuaala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa aliwataka Wazanzibar kuungana pamoja na kuendelea kumuunga mkono Rais Ali Mohamed Shein hususani katika jitihada zake za kuimarisha ushirikiano na mataifa ya kigeni.

Balozi Ramia alisema katika siku za hivi karibuni kumeibuka hofu isiyo na sababu kuhusu ziara ya Mfalme Qaboos Said Al-Said na kueleza kuwa katika mazungumzo baina ya Viongozi hao wawili hakukuwa na suala la kisiasa lililojadiliwa badala yake ni masuala ya uimarishaji wa ushirikiano wa maendeleo ya wananchi.
“Kuna minong’ono kuwa Zanzibar ilibanwa na mfalme Qaboos Said Al-Said kuhusu hali ya kisiasa, jambo hilo hakuna na badala yake Viongozi ho walijadili masuala ya ushirikiano na hatua zinazopaswa kuchuliwa ili kuharakisha maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Gavu (kulia) akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari kuhusu tathimini ya ziara ya Ujumbe wa Mfalme wa Oman, Qaboos bin Said Al-Said uliozuru Zanzibar hivi karibuni. Kushoto ni Mshauri wa Rais wa Zanzibar katika masuala ya Ushirkiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi Mohamed Abdiwawa.
Baadhi ya Waandishi wa vyombo vya habari wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Gavu (kulia) akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari kuhusu tathimini ya ziara ya Ujumbe wa Mfalme wa Oman, Qaboos bin Said Al-Said uliozuru Zanzibar hivi karibuni.