Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa ameuagiza uongozi  Wakala wa Barabara (TANROADS), Makao makuu kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja  wanaweka mzani mwingine wa kuhamishika katika eneo la mzani wa Makambako ili kuweza kutatua  changamoto ya msongamano wa magari katika eneo hilo.
Naibu Waziri huyo ametoa agizo hilo mkoani Njombe, mara baada ya kufika katika mzani huo ambapo amejionea changamoto zake na kusisitiza kuwa,  kuongeza mzani wa kuhamishika katika eneo hilo kutasaidia kupunguza kero hiyo ya msongammano wakati Serikali ikitafuta ufumbuzi wa kudumu wa kujenga mzani mwengine katika eneo hilo.
"Naagiza TANROADS Makao makuu mfanye kila linalowezekana  ndani ya mwezi mmoja mlete mzani wa  kuhamishika hapa Makambako,  tunataka tutoe huduma ya haraka kwa madereva  ili  pasiwe na  msongamano katika eneo hili", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Amewaonya wale madereva wote wanaotumia kisingizio cha uwepo wa foleni  katika mzani  huo kwa kufanya mambo yao binafsi kuacha mara moja tabia hiyo, kwani ikibainika kwa dereva yeyote ambae ameshapatiwa huduma lakini bado ameegesha gari lake katika eneo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria dhidi yake.
Ameagiza Taasisi zote zinazotoa huduma katika mzani huo kushirikiana na kuandaa maoni yao kuhusu namna ya kupunguza msongamano katika mzani huo na kuyawasilisha Wizarani ili yaweze kufanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Njombe, Mhandisi, Yusuph Mazana, ametaja baadhi ya changamoto zilizopo katika Mzani huo kuwa ni kuharibika kwa mzani mara kwa mara kutokana na mzani huo kuwa ni wa siku nyingi na kuwepo na muingiliano wa huduma kutoka Taasisi mbalimbali za serikali kama  Uhamiaji, Polisi na TRA.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya magari kuegeshwa nje ya maeneo ya mzani baada ya kupima na hivyo kusababisha msongamano wa magari yanayotakiwa kuingia ndani ya eneo la mzani kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji au kufanya taratibu nyingine.
Naibu Waziri Kwandikwa amemaliza ziara ya kikazi katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambapo alipata fursa ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali   inayotekelezwa na Sekta yake.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na wafanyakazi wa mzani wa Makambako, wakati alipotembelea mzani huo kufahamu changamoto wanazozipata katika utendaji wao wa kazi, Mkoani Njombe. 
Muonekano wa mzani wa Makambako, mkoani Njombe, wenye uwezo wa kudhibiti uzito wa magari makubwa yanayozidi 3500kg (tani 3.50). 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...