Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia viongozi na wananchi wa Dodoma baada ya kutua kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akitoka uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam Januari 16, 2017 ikiwa ni uzinduzi wa Safari za ndege za Shirika hilo kati ya viwanja viwili hivi.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.
Akizindua safari hizo leo (Jumatatu, Januari 16, 2017) amesema safari hizo zitawezesha wafanyabiashara na wananchi wengine kutoka Dodoma na kwenda katika maeneo mengine kwa urahisi.

Amesema kuanzishwa kwa safari hizo ni moja ya utekelezaji wa ahadi za Mheshimiwa Rais, Dkt.  John Magufuli za kufufua ATCL na kuboresha usafiri wa anga nchini.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa umma, wafanyabiashara na wananchi wa Dodoma kutumia ndege hizo kwa safari za kwenda katika maeneo mbalimbali kwani ni za uhakika na gharama zake ni nafuu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea mfano wa Boarding Pass kutoka kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mahandisi Edwin Ngonyani kabla ya kusafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere, Dar es salaam kwenda Dodoma Januari 16, 2017. Alikuwa akizindua safari za ndege za shirika hilo kati ya viwanja viwili hivyo.

“Tuna ndege nzuri. Tuzitumie kwenda katika maeneo mengine kwani gharama zake ni nafuu. Kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ni sh. 165,000, kwenda na kurudi ni  sh. 299,000,” amesema.

Amesema ndege nyingine kama hiyo inatarajia kuwasili nchini Juni mwaka huu jambo ambalo litaongeza idadi ya safari za ndege hizo nchini na maeneo mengine ya nchi jirani.
Naye Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma kutumia vizuri fursa hiyo ya safari za ndege za ATCL kwa kuwa utawawezesha kusafiri kwa muda mfupi tofauti na vyombo vingine vya usafiri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Jordan Rugimbana ameshukuru kwa uanzishwaji wa safari hizo kwa kuwa zitarahisisha kutoka katika Makao Makuu ya nchi na kwenda katika mikoa mingine nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisafiri kwa ndege ya Bombardier Q400 ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kutoka uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere kwenda Dodoma Januari 16, 2017. Alikuwa akizindua safari za ndege za ATCL katika viwanja viwili hivyo. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Leonard Chamuriho.

Naye Waziri Mkuu Mstaafu Mzee John Malecela ameupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa namna anavyofanya kazi. Amefurahishwa na uanzishwaji wa safari hizo.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa ATCL. Kapten Richard Shaidi ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa ujio wa ndege hizo na kwamba hiyo ni moja ya mikakati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ya kufufua ATCL.
“Hivi karibuni tunaanza kwenda nchi jirani. Mwakani tutapata ndege nyingine kubwa itakjayokuwa inafanya safari za masafa ya kati na ya mbali.

Naipongeza Serikali kwa kutoa ahadi na kuitekeleza kwani kutoa ahadi ni jambo rahisi ila utekelezaji wake ndiyo kazi. Lakini Serikali imeweza,” amesema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ​ baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akitoka uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam ikiwa ni uzinduzi wa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kati ya viwanja viwili hivyo, Januari 16, 2016. Wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijan, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Bw. Emmanuel Korosso amesema hivi karibuni shirika hilo linatarajia kuanza safari za kwenda katika miji ya Tabora, Songea, Mtwara, Mpanda, Mafia na Jiji la Tanga.
Akizungumzia kuhusu safari za Dodoma amesema zitafanyika mara mbili kwa wiki, siku ya Ijumaa na Jumatatu. Hata hivyo wanatarajia kuongeza safari hapo baadae.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...